RAIS SAMIA KUFANYA ZIARA YA KIKAZI NCHINI ANGOLA

RAIS SAMIA KUFANYA ZIARA YA KIKAZI NCHINI ANGOLA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaondoka nchini leo tarehe 31 Julai, 2026 kwenda nchini Angola kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Angola, Mheshimiwa João Manuel Gonçalves Lourenço.

Akiwa nchini humo, Rais Dkt. Samia na mwenyeji wake, Rais Lourenço, watashiriki katika hafla ya uzinduzi wa hospitali ya rufaa iliyopewa jina la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, iliyopo jijini Luanda.

Hafla hiyo pia itahudhuriwa na familia ya Baba wa Taifa ikiongozwa na Mama Maria Nyerere.

Aidha, Rais Dkt. Samia atafanya mazungumzo na Rais Lourenço na kushiriki hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Wake wa Marais wa Afrika kwa lengo la kuchangisha fedha za utekelezaji wa shughuli za kijamii na kiuchumi za uwezeshaji wa wanawake na vijana.

Ziara hiyo ni mwendelezo wa kuimarisha uhusiano wa kihistoria na wa kindugu kati ya Tanzania na Angola, uliojengwa tangu enzi za harakati za ukombozi wa Bara la Afrika.