MHE:JANETH PINDA AIBANA SERIKALI KUJENGA KIWANDA CHA DAWA

MHE:JANETH PINDA AIBANA SERIKALI KUJENGA KIWANDA CHA DAWA

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Katavi, Mhe. Janeth Pinda, ameiomba serikali kuweka kipaumbele katika bajeti inayokwenda kutekelezwa kwa kujenga kiwanda cha dawa , ili kukabiliana na uhaba mkubwa wa dawa. 

Akizungumza wakati wa kuchangia hoja bungeni jijini Dodoma, Mhe.  Janeth Pinda amesema kuwa mapinduzi makubwa yaliyofanywa na serikali katika kujenga miundombinu ya hospitali na vituo vya afya  hayatokuwa na tija kama wananchi watakosa dawa pindi wanapofuata matibabu.

Mhe.Janeth Pinda amefafanua kuwa, kuanza kutumika kwa mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote kutasababisha wimbi kubwa la wananchi kujitokeza kupata huduma za matibabu, hatua itakayoongeza uhitaji wa dawa kwa kiasi kubwa.

"Tumejengewa hospitali, tumejengewa vituo vya afya ndani ya mkoa Lakini watu wetu watakumbwa na uhaba mkubwa wa madawa kwa sababu sasa tunaenda kwenye bima ya afya na wengi watahitaji huduma, Kukiwa na changamoto ya dawa, wananchi watakosa huduma na bima itashindwa kufanya kazi vizuri," amesema Mhe. Janeth Pinda

Aidha  Mhe.Janeth Pinda ameipongeza Wizara ya Afya kwa kuonyesha nia thabiti na kulipa kipaumbele kikubwa suala la Bima ya Afya kwa Wote, Amesema hatua hiyo ni ukombozi mkubwa kwa afya za Watanzania wanyonge.