GHANA YAKUBALI PENDEKEZO LA KUONGEZA MUDA WA URAIS

GHANA YAKUBALI PENDEKEZO LA KUONGEZA MUDA WA URAIS

Serikali ya Ghana imekubali pendekezo la kuongeza muda wa muhula wa rais kutoka miaka minne hadi miaka mitano, pamoja na kupunguza umri wa chini wa kugombea urais hadi miaka 35.

Rais John Dramani Mahama aliunda kamati mwaka jana kwa ajili ya kutathmini na kupendekeza mabadiliko katika katiba ya nchi hiyo,Kamati hiyo iliwasilisha ripoti yake ya mwisho jana Alhamisi.

Waziri wa Sheria, Dominic Ayine, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, "serikali imekubali pendekezo la kuongeza muda wa muhula wa rais kutoka miaka minne hadi miaka mitano."

Kamati hiyo pia ilipendekeza muda wa bunge uongezwe kutoka miaka minne hadi miaka mitano ili uendane na muhula wa rais.

Ingawa kamati ilipendekeza umri wa chini wa wagombea urais upunguzwe hadi miaka 30, Ayine ameeleza kuwa serikali imeamua kuupunguza hadi miaka 35 badala yake.

Mabadiliko hayo yatahitaji kuidhinishwa kupitia kura ya maoni ya kitaifa itakayofanyika mwaka 2027. Ili yapitishwe, yatapaswa kufikia viwango vilivyowekwa vya ushiriki wa wapiga kura pamoja na idadi inayohitajika ya kura za kuunga mkono.