DIWANI WA KATA YA MAKANYAGIO ATOA MAAGIZO KWA MTENDAJI MPYA

DIWANI WA KATA YA MAKANYAGIO ATOA MAAGIZO KWA MTENDAJI MPYA

Diwani wa Kata ya Makanyagio, Manispaa ya Mpanda, Erick Lazaro Katakwa, amemtaka Mtendaji mpya wa kata hiyo kuibua na kuendeleza miradi ya maendeleo itakayochochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Akizungumza katika kikao cha makabidhiano kati ya Mtendaji aliyekuwa akihudumu awali na Mtendaji mpya, Diwani Katakwa amesisitiza umuhimu wa kuendeleza miradi iliyopo pamoja na kuanzisha mingine mipya yenye tija kwa wananchi. Miongoni mwa miradi aliyotaja ni mradi wa Soko la Samaki lililopo Makanyagio, Mtaa wa Kachoma.

Amesema ushirikiano kati ya viongozi na wananchi ni msingi muhimu wa kufanikisha maendeleo ya kata hiyo, huku akiahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa mtendaji mpya ili kuhakikisha miradi mbalimbali inatekelezwa kwa ufanisi.

Katika hatua nyingine, diwani huyo amewahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika Juni 6 pamoja na ufunguzi wa Kliniki ya Upatikanaji wa Hati za Nyumba utakaofanyika Juni 9, akieleza kuwa matukio hayo yatasaidia kuimarisha maendeleo na ustawi wa wananchi wa Kata ya Makanyagio.

Kwa upande wao, watendaji hao wameeleza kuwa wameupokea uhamisho huo kwa mtazamo chanya, wakibainisha kuwa ni sehemu ya utumishi wa umma unaolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Pia wameahidi kushirikiana kikamilifu katika kutekeleza wa majukumu yao mapya kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya kata husika.

Kikao hicho kilihitimishwa kwa viongozi na watumishi kuwatakia kila la heri watendaji hao katika majukumu yao mapya huku wakisisitiza umuhimu wa ushirikiano, uwajibikaji na mshikamano katika kuharakisha maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.